Monday, May 20, 2013

HAKI YA KUKATA RUFAA TANZANIA

SWALI: Rufaa ni nini? Sheria gani inahusika na masuala ya Rufaa Tanzania?

DENIS MARINGO: Rufaa ni wasilisho mahakamani ambapo upande fulani usioridhika na hukumu iliyotolewa huiomba mahakama ya juu kupitia upya na kurekebisha ama kutengua hukumu husika.
Zipo heria kadhaa zinazotoa haki ya kukata rufaa. Sheria hizi zaweza kua zile zinazohusu kesi zote kwa ujumla nchini, kama ilivyo heria ya Mahakama za Mahakimu ya mwaka 1984. chini ya sheria hii maamuzi ya mahakama za Mwanzo hukatiwa rufaa mahakama za Wilaya ama hakimu Mkazi.Maamuzi haya nayo yaweza kukatia Rufaa Mahakama Kuu.

Uamuzi wa Mahakama Kuu unaweza kukatiwa Rufaa Mahakama ya Rufaa ambapo ndipo ukomo ulipo. Mifano ya maamuzi muhimu yaliyofika Mahakama ya Rufaa na kutoa ufafanuzi wa kina wa heria husika ni pamoja na Bi. Hawa Mohamed v. Ally Sefu [1983] TLR 32 ambayo ilihusika na mgawanyo wa mali ndoa inapovunjia pamoja na shauri la Kukutia Ole Pumbun [1994] lililohusika na mashtaka yanayoletwa dhidi ya Serikali. Angalia pia hukumu katika rufaa za Daudi Pete; Lohay Akooonay, Agnes Doris Liundi na nyinginezo muhimu.

Muhimu kukumbuka kuwa haki ya Kukata rufaa ni ya Kikatiba kuitia ibara 13(6)(a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.



Monday, May 13, 2013

FIDIA KWA MADHARA YATOKANAYO NA UZEMBE WA MTU MWINGINE

SWALI: Je, naweza klushtaki iwapo A anafanya uzembe inaosababisha madhara kwangu au mali yangu?

NDIYO: Kama mna mkataba unaweza kushtaki kwa kutumia vipengele vya ukiukwaji mkataba. Unaweza pia kuleta mashtaka sambamba na hili, ama pia kama huna mahusiano ya maktaba na huyo aliyekutenda, kwa kutumia Sheria za Madhara ziitwazo 'Torts'. Misingi ya makosa ya uzembe imefafanuliwa katika hukumu maarufu ya Donoghue v. Stevenson na nyinginzeo kama Blythe v. Birmigham Water Works ambapo Jaji Bwanyenye Aderson (Lord Alderson) alifafanua nini maana ya uzembe kisheria:

"Kutokufanya jambo ambalo mtu mwenye akili ya kawaida angepaswa kulifanya ama kufanya jambo ambalo mtu mwenye akili ya kawaida angeepuka asilifanye"

Na pia angalia hukumu ya Lord Esher katika Le Lievre Dhidi ya Gould [1891] 1 Q.B. 491 iliyohukumiwa na Kitengo cha Utoaji haki cha Malkia wa Uingereza (Q.B.D)

NAFUU YA FIDIA KWA KUBAMBIKIZIWA KESI NA KUSHTAKIWA MAKUSUDI

SWALI: Je, naweza kumshtaki raia mwenzangu, polisi ama ofisa anayenibambikizia kesi kwa lengo la kunikomoa na hatimaye nikashtakiwa jinai kwa makusudi na hila japo sikuwa na hatia yoyote?

DENIS MARINGO: Ndiyo waweza. Jambo hili limefafanuliwa mahali pengi na pia katika hukumu ya Festo Dhidi ya Mwakabana (1971) HCD n.417 na ile ya Hosia Lalata Dhidi ya Gibson Zumba Mwasote [1980] TLR 154. Kesi za kubambikiziana ama kukomoana chimbuko lake ni hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Kibwanyenye ya Uingereza (House of Lords) katika shauri maarufu la Herniman v. Smith [1938] A.C. 305

TARATIBU ZA KUISHTAKI SERIKALI YA TANZANIA MAHAKAMANI

SWALI: Je, mimi kama Mtanzania naweza kuishtaki Serikali yangu hii ya Tanzania kama naona imenitenda jambo baya ama imekiuka yenyewe Sheria zetu na Katiba ya nchi yetu?

DENIS MARINGO: Ndiyo, waweza. Hata hivyo umeshatamka mwenyewe 'Serikali'. Kuishtaki dola si jambo jepesi lakini mara kwa mara linafanyika na hata serikali kuonekana imevunja sheria zake yenyewe ama  Katiba.Taratibu za kuishtaki Serikali zimefafanuliwa katika Katiba na Sheria nyinginezo kama Governnment Proceedings Act. Na pia kuna Sheria kama The Basic Rights and Duties Enforcement Act, 1994 ama nyinginezo kama Sheria ya Mwenendo wa Kesi za Madai (Civil Procedure Code Act). Watafute wanasheria wakusaidie kwa ufafanuzi.  Muhimu hata hivyo ni kuwa ujue unachoshtakia kama kitakubalika na mahakama, ujue ni mahakama ipi utapeleka jambo lenyewe na pia utoe taarifa (notis) ya awali kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kulingana na misingi iliyoanishwa katika hukumu za  Peter Ngh'omango dhidi ya Gerson Mwangwa [ 1993] TLR  na ile ya Kukutia Ole Pumbun na Mwenzake Dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Tanzanial; ile ya mfanyabiadhara Lucas Matafu Dhidi ya Mheshimiwa Mustafa Songambele [1976] LRT n.10 ; na nyinginezo kadhaa. Zamani ulipaswa kuomba idhini Serikali yenyewe kuwa unakusudia kuishtaki lakini jambo hili lilibatiliwa na Mahakama kwa kuonekana kukiuka Katibam na hasa ibara ya 13(6)(a) .

MWAJIRI AWEZA KUWAJIBIKA KWA MAKOSA YA MWAJIRIWA?

WEWE: Bwana Sheria. Je inawezekana kweli kumshtaki mwajiri kwa jambo linalota madhara kwa mwingine ambapo mwajiri mwenyewe hajafanya kosa ila limefanywa na mwajiriwa? Mathalani, Je naweza kuumia kwenye basi nikamshtraki mmiliki kwa kutokuwa makini katika kuajiri dereva mzembe na asiye na taaluma, kiwango au mafunzo?

DENIS MARINGO: Swadakta. Hilo lawezekana japo si mara zote kwa vile lina misingi na mipaka yake. Kisheria nadharia hii inajulikana kama 'Vicarious liability' (liability of the Master by the Acts/Omissions) of his Servant. Wamombo wanaamanisha hapa kuwa 'Uwajibikaji kisheria wa Mwajiri/Bwana katika makosa ya Mwajiriwa/Mfanayakazi. Enzi za Ukabaila ama Utumwa tungeweza kuongezea 'Mtwana' pia. Kwa Tanzania nadharia hii ilifafanuliwa vema na Mahakama Kuu katika hukumu ya Anglina v. Nsubuga na Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba (1971) HCD n. 190

HUKUMU YA DAUDI PETE [1993] TLR NA MISINGI YA DHAMANA KMA HAKI YA KIKATIBA

WEWE: Hii hukumu ya Daudi Pete nimeisikia hapa na pale. Nini kitu hiki?

DENIS MARINGO: Hukumu hii ya Daudi Pete [1993] TLR ilitolewa mwanzoani mwa miaka ya tisini na na mahakama zetu za juu inahusika na utolewaji wa Dhamana kama haki ya Kikatiba. Ilifafanuliwa kupitia hukumu hii kuwa Dhamana ni haki ya Kikatiba na isinyimwe pasipo sababu nzito na za msingi kwa sababu Katiba inatamka kuwa mtuhumiwa wa kosa anapaswa kuhesabika hana hatia hadi anapothibitishwa na mahakama yenye mamlaka husika kuwa ametenda kosa hilo, ispokuwa pia kwa makosa mazito na makubwa ambayo utolewaji wake umewekewa kigingi na Sheria husika. makosa haya ni kama kuua kwa kukususia (murder) na uhaini (treason).

HUKUMU YA AGNES DORIS LIUNDI INA UMUHIMU GANI TANZANIA?

WEWE: Nimesikia sikia kutajwa kwa hukumu ya Agnes Doris Liundi. Inahusika na nini?

DENIS MARINGO: Zipoi Hukumu mbili za Agnes Doris Liundi na zote mbili zina umuhimu mkubwa katika masuala ya Sheria za Jinai Tanzania. Unazungumzia ipi kati ya hizo. Basi niweke tu mambo sawa kwa kusema kuwa zote mbili zilihukumiwa na Mahakama za juu Tanzania japo zinatofautiana kwa mamlaka. ya Kwanza ilihukumiwa na Mahakama Kuu na hiyo inaitwa JAMHURI v. AGNES DORIS LIUNDI na ya pili ikawa ni rufaa ya Bibi Agnes mbele ya Mahakama ya Rufaa akiomba hukumu dhidi yake itenguliwe. Hii ya Pili iko sahihi kama utaitaja AGNES DORIS LIUNDI v. JAMHURI. Kumbuka, kisheria yule anayewasilisha malalamika kama mshtaki wa awali ama mkataji rufaa jina lalke hutajwa mwanzao na yule anayeshtakiwa ama kukatiwa rufaa dhidi yake hufuatam na ndiyo mantiki ya tifauti hii hapo Juu. Turejee katika swali lako.

Bibi Agnes Doris Liundi alikuwa mke wa Balozi Liundi na mwishoni mwaka 1979 aliwaua wanawe wadogo watatu-kati ya wanne- kwa kuwatumbukiza majini nyumbani kwake Keko, Temeke,  Dar es Salaam baada ya kuonekana kuwa amechanganyikiwa kwa atahri za mgogoro wa unyumba na mumewe. Jamhuri ikamshtaki kwa makosa ya kuua kwa kukusudia na hii ndiyo kesi iliyokuwa Mahakama Kuu ya Tanzania na ikatolewa hukumu na Jaji Lewis Makame amabye hakukubaliani na utetezi wa Bibi Liundi kuwa alikuwa akiugua wazimu (Insanity) alipotenda kosa hilo. msingi wa utetezi huu ni hukumu maarufu ya Uingereza iitwayo M'naughten ambayo inatumika kote ulimwenguni.

Ndipo alipokata rufaa mahakama ya Rufaa ambapo mahakama hiyo pia ikakataa utetezi wake. Kwa hivyo basi hukumu hii ni muhimu kuelewa dhana kadhaa kama vile a kuua kwa kukusudia, kuua bila kukusudia, utetezi wa wazimu (insanity plea) na nafasi ya ushahidi wa kitabibu (Medical evidence) katika kesi za jinai.

ZUIO LA MAHAKAMA (INJUNCTION) NI KITU GANI? (LUCAS MATAFU v. MUSTAFA SONGAMBELE)[1977] LRT 10

WEWE: Nini maana ya Injunction. Tusaidiane katika lugha yetu ya Taifa.

DENIS MARINGO: Una maana gani uaposema lugha ya Taifa. Nasema hivi kwa vile KIINGEREZA ni Lugha ya Taifa pia kwa mujibu wa Katiba yetu. Ningekujibu kwa Kiswahili ama Kiingereza kwa vile zote ni lugha za Taifa-Kwa mujibu wa Katiba! Nimekusoma pengine unahitaji maelezo Kiswahili.

Injunction ni amri ya mahakama ambao 'inazuia' jambo fulani lisifanyike na yule 'anayetaka kulifanya'.
honde chonde, zingatia sana hicho nilichoki-bold na kukupigia mstari kwa maana msisitizo. Wapo Wana sheria wenye kufikiri kimakosa kuwa injunction ni amri ya mahakama. Hii haitoshi. Haitoshi kwa sababu amri yaweza kuamru jambo lifanyike ama lisifanyike. Injunction haifiki huko. Injunction ni kitu cha Magharibi tu, hakiendi Mashariki. Ni kitu cha Kushoto-kamwe hakielekei kuumeni. Nina maana gani?

Kusema kweli nashukuru sana hekima za hayati Jaji Lameck MFALILA kwa uamuzi ulijaa busara kubwa katika shauri alilohukumu la Lucas Matafu v. Hon. M. M. Songambele[1977] LRT 10


Hata siku moja, na kamwe, Injunction haijawahi kumaanisha amri ya kufanyika jambo. injunction hukata tu kwa kuzuia. Ki-msingi injunction inakuwa na maana tu pale inapokidhi mambo haya mawili (la tatu na muhimu zaidi na ambalo lingepaswa kuwa la kwanza, silitaji hapa kwa sasa):

(1) Injunction itatolewa na mahakama kama kile kinachotakwa kizuilike kufanyike bado hakijafanyika. Maana yake ni kuwa utakuwa mwendawazimu kuomba injunction kumzuia mtu asitangaze matokeo ya uchaguzi kama tayari kura zimechakachuliwa na matoke yamrtangazwa ama kuzuia nyumba isiuzwe ama kubomolewa wakati haya yameshafanyika!

(2) Ewe Wakili iombe Mahakama itoe Injunction 'KUZUIA JAMBO LISIFANYIKE' na si 'KUSHINIKIZA JAMBO LIFANYIKE'.  Injunction ni kuzuia na si kuamrisha!

HUKUMU YA HAWA MOHAMED v. ALLY SEFU [1983] TLR 32 INAHUSIKA NA NINI?

WEWE: Bwana Maringo. Nime-google kuhusu sheria za Tanzania na kila mahali nakutana na majina Hawa Mohamed v. Ali Seif. Hiki ni kitu gani sasa? Nifungue macho.

DENIS MARINGO: BI. HAWA MOHAMED v. ALLY SEIF [1983] TLR 32 Ni hukumu muhimu na maarufu kuliko zote pale linapokuja suala la migogoro ya wana-ndoa wanaotaka kutalikiana na pia suala zima la ugawanaji mali pale mahakama inaporidha talaka itolewe na ndoa hiyo ihesabike kwamba imeshindwa kuhimi mikikimikiki ya kutoelewana. nazungumzia hapo tamu inayogeuka kuwa shubiri baadaye.

Hukumu huu ilitolewa mwaka 1983 na Jopo la Majaji Watatu wa Mahakama ya Rufaa Tanzania (Jaji Mkuu Nyalali, kama alivyokuwa wakati ule, Jaji Lewis Makame na Jaji Robert Kisanga). Mengi yalizungumzwa humo na kinachoskikitisha hata baadhi ya wanasheria wameilewa vibaya hukumu hii kwa kutoisoma kwa umakini neno kwa neno, aya kwa aya. Inatosha tu kusema kuwa kikubwa kilichoelekezwa hapo ni kwamba mama wa nyumbani anastahili kupata mgawo katika mali iliyochumwa na wanandoa hata kama kazi alizofanya ni za nyumbani tu na mumewe haijalishi alikuwa akikesha akirusha ndege, katika vikao vya mawaziri, kwenye dili kubwa ama safari za ki-biashara ana kazi nyinginezo, iweza kitaalam ama za suluba. Nikumbushe tena, jambo hili lisieleweke kijumla jumla tu hivyo, mahakama ilitoa ufafanuzi zaidi katika hili na sitaweza kutazungumza yote hapa.

Kesi hii ni muhimu kwa vile Mahakama hii ikiwa ni ya Juu zaidi Kikatiba na ambayo hukumu zake zapaswa kufuatwa na mahakame zote chini yake (katika tafsiri ya sheria husika). Ndiyo kusema,Jaji wa Mahakama Kuu, Hakimu wa Mahakama ya Wilaya au Ilala na wengineo wanatarajiwa kuzingatia msingi uliwekwa hapo.

SHERIA ZA JINAI TANZANIA


WEWE: Sheria zipi zinatawala masuala ya jinai Tanzania?

DENIS MARINGO:  Zipo Sheria kadhaa lakini Sheria ziliyo Kuu na muhimu zaidi kwa masuala ya jinai na Tanzania nya Kwanza ni Ile iitwayo Penal Code (cap. 16) kama ilivyozoeleka kimombo. Kwa Kiswahili Sheria hii huitwa KANUNI YA ADHABU na hata kama utasema tu SURA YA 16 Ya Sheria za Tanzania mwanasheria yeyote atakuelewa na hata mahakama inayosikiliza kesi yako ya jinai ama nduguyo itakuelewa pia.   Sheria hii inaumba makosa takribani yote unayoyajua ni jinai (wizi, mauaji, ubakaji, uhaini na kadhalika) na pia inatamka adhabu kwa takribani kila kosa inaloliumba humo.

kama nilivyodokeza zipo sheria nyinginezo pia.Mathalani, SHERIA YA MWENENDO WA MAKOSA  JINAI, kimombo ikifahamika kama CRIMINAL PROCEDURE ACT, ni muhimu sana ewe Mtanzania ukainunua na ukaisoma na kuilewa. Kwa nini?  taratibu za wewe ama nduguyo kukamatwa ama kuhojiwa na polisi ama mamlaka za dola zimo humo. Utoaji dhamana kwa watuhumiwa umefafanuliwa humo. Polisi anapaswa afuate yale yaliyoelekezwa humo pale anapotaka kukusaili ama kukufanyia upekuzi nyumbani ama katika gari lako na mahali popote nchini. yamo mengi zaidi ya hayo katika sheria hii ambayo falsafa yake ilikuwa ni kumlinda raia na haki zake pale anapokabiliwa na tuhuma za jinai na pia kudhibiti matumizi yasiyofaa ya utumiaji nguvu za dola.

Na tena nimefafanua kuwa zipo sheria zaidi kama ile ya Minimum Sentemcing Act, 1972 ambayo inaweka misingi ya Utoaji adahabu kwa wale waliotiwa hatiani. je uende gerezani/ chuo cha mafunzo na kwa muda gani. yamo humo. Utandikwe mijeledi ama la? Hilo ni kosa lako la kwanza, je utastahili kutumikia adhabu sawa na mtu aliyetenda kama wewe lakini kakubuhu katika jinai? Yamefafanuliwa humo.

Na pia tena takribani kila sheria nyinginezo huwa zinatoa adhabu katika kifungu kimoja, viwili au vitatu hivi. heria ya Uchaguzi ya mwaka 1985 imebeba jinai katika amsuala ya kutaka kuvuruga uchaguzi na kadhalika. Sheria za Filamu zina vifungu vya jinai kuhusu uonyesha picha za ngono. Sheria za barabarani zina jinai kuhusu uendeshaji magari hatarishi ama kuendesha bila bima ya lazima. Sheria za utangazaji zaweza na hakika zina jinai kuhusu uchochezi. Sheria za kuabudu vile vile vile Sheria za Elimu zina jinai kuhusu wizi wa mitihani. Sheria za Benki zina jinai kuhusu masuala ya utakatishaji fedha na kadhalika. Hii ni mifano tu.

SHERIA KUHUSIANA NA NDOA TANZANIA NI ZIPI?


WEWE: Sheria zipi zinatawala masuala ya ndoa Tanzania?

DENIS MARINGO:  Zipo Sheria kadhaa lakini Sheria iliyo Kuu na muhimu zaidi kwa masuala ya ndoa na familia inaitwa Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971. Inarejewa pia kama Sheria namba 5 ya mwaka 1971 na ni maarifu zaidi miongoni mwa wanasheria ndani na nje ya mahakama kwa jina la Law of Marriage Act, 1971. Sheria hii moja kwa moja inatawala ndoa za Kiseerikali na zile za kidini na pia zile za kimila kama zilivyoanishwa katika matangazao mawili muhimu ya Serikali ya mwaka 1963 kuhusiana na ndoa, talaka na ugawanaji mali na wato kimila. Kwa Ndoa za Kiislam, Sheria za Kiislam zinafuatwa na kuhesjimiwa na mahakama kama wanandoa husika wamefunga ndoa kwa kufuata imani ya dini hii. 

KATIBA YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, 1977


WEWE: Katiba yetu ilitungwa lini?

DENIS MARINGO: Katiba inayotumika Tanzania sasa imekuwepo tangu mwaka 1977.

KUHUSU MIMI

WEWE: Tupe wasifu wako kifupi.

MIMI : Naitwa Denis Maringo. Ni Mtanzania wa kuzaliwa.

SHERIA ZA ARDHI TANZANIA

WEWE: Sheria zipi zinahusiaka na Ardhi Tanzania.

DENIS MARINGO:Inategemea unazungumzia ardhi ipi na iko wapi ama jambo gani kuhusiana na ardhi husika. Kifupi naweza tu kukuridhisha kuwa Ardhi si suala la Muungano. tanzania bara wana Sheria za ardhi na Zanzibar pia wanazo zao kwa masuala ya huko. Kimsingi, hata hivyo, kwa Tanzania bara, sheria maarufu ya ardhi ya mwaka 1923 (Land Ordinance) haipo tena. tangu mwaka 1999 Bunge lilitunga Sheria mbili muhimu katika jambo hili. Sheriaya Ardhi namba 4 ya mwaka 1999 inatawala masuala muhimu na ya ujumla ya ardhi Tanzania. Sheria namba 5 ya mwaka 1999 inahusika zaidi katika ardhi iliyo katika himaya ya Kimila ama Vijiji. Sheria Nyingine muhimu ni Sheria ya Uandikishaji Ardhi. Je ni hizi tu? usipotoke. Umetokea mgogoro wa ardhi unakimbilia wapi na utatuzi unakuwaje? Ipo sheria katika hili-nayo yaitwa Sheria ya Mahakama za Adhi ya mwaka 2002.

Kwa vile pengine wewe si Mwanasheria usijiridhishe kwamba umeshajua sasa sheria hizi kwa kusoma hicho nilichodonia hapo juu. Wamombo wangesema 'that's just a tip of an iceberg!.  Basi nakusihi ndugu yangu tafuta mwanasheria makini katika ufafanuzi wa masuala haya ili usije ukabaini imepoteza haki yako kwa kutowatafuta wale waliofundishwa kukusaidia wewe. Je, ukiugua Malaria, T.B au gonjwa lolote waweza kujipima na kujitibu? Kama hasha, basi naamini umenielewa. Twende mada nyingine!

KUHUSU BLOGU HII

Kuelimisha Umma wa Tanzania kuhusiana na Sheria za nchi hii na hukumu muhimu zilizotafsiri sheria hii.

Kuwasilisha hukumu hizi kwa lugha ya KISWAHILI kwa kutumia tafsiri zangu mwenyewe na pia tafsiri yako wewe Msomaji na wapenzi wengine watakaofuatilia hapa.

Kuwasilisha makala/maandiko niliyowahi kuandika katika Vyuo vikuu nilikosomea Taaluma hii na marejeo niliyoawahi kujisomea nikiwa katika nchi hizi tatu (Mlimani-anzania,  Marekani na Uholanzi)

Kukosoa, kwa ushirikiano na watanzania wenzangu, mapungufu yaliyomo katika Sheria zetu ili kujenga taifa lnye utawala bora wa sheria, kuondoa urasimu na ukiritimba wa kisiasa, kiutawala na kuimarisha demokrasia, haki na fursa kayika nyanja zote kwa Watanzania wote bila kujali umri, jinsi, dini, kabila, nasaba, rangi ya mtu, elimu, mahali anapoishi, hali ya kiuchumi, shughuli aifanyayo na kadhalika.

Kuwatambua watanzania waliotoa mchango muhimu katika kuimarisha dhana ya uytawala bora na utawala wa sheria na poia utetezi wa haki za binadamu nchini.

Kufanya mambo mengine yoyote ambayo yatachochea malengo haya hapo juu kwa kuzingatia kutovunja Sheria zisizokinxana na misingi ya katiba na haki za binadamu.

TUANZE KAZI!!!